Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

National Ranching Company Limited - NARCO

Karibu

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Kwa niaba ya Kampuni ya Ranchi za Taifa Ltd (maarufu kama NARCO), mzalishaji pekee wa nyama pendwa ya Kongwa Beef nakukaribisha sana katika tovuti yetu hii mahsusi. Kupitia tovuti hii utaweza kupata taarifa mbalimbali na za uhakika zinazoihusu Kampuni ya Ranchi za Taifa na juhudi zetu katika kuongeza ufugaji wenye tija na uendelezaji wa biashara ya mazao ya mifugo hapa Tanzania na nchi za nje. Kupitia tovuti hii utapata taarifa sahihi juu ya ranchi zetu zinazopatikana katika mikoa tisa hapa Tanzania. Utapata pia taarifa za aina mazao yanayopatikana katika ranchi na jinsi unovyoweza kufanya biashara nasi. Tovuti hii itatoa matangazo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mifugo, vitalu vya kufugia na zabuni mbalimbali. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, tovuti hii itakupa fursa ya kuwasiliana nasi, kutoa mrejesho, kutoa dukuduku na maoni juu ya Kampuni ya Ranchi za Taifa. Nakushukuru sana kwa kuamua kututembelea katika ofisi yetu hii mtandaoni. Nakukaribisha tena na kukuomba uwashirikishe wengine.

Kampuni ya Ranchi za Taifa ilianzishwa rasmi mwaka 1975 baada ya kubadilishwa jina kwa iliyokuwa National Agricultural Company (NACO) ambayo ilikuwepo tangu mwaka 1968. Kampuni ya Ranchi za Taifa inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kampuni ina jukumu kubwa la kuzalisha mifugo kwenye ranchi hasa ng’ombe wa nyama kwenye ranchi 15 zilizosambaa katika mikoa tisa hapa Tanzania.

Utazikuta ranchi za NARCO Dodoma (Kongwa), Morogoro (Dakawa and Mkata), Pwani (Ruvu), Tanga (Mzeri Hill), Kilimanjaro (West Kilimanjaro), Kigoma (Uvinza), Kagera (Kikulula, Mabale, Kagoma, Kitengule, Misenyi na Mwisa II), Rukwa (Kalambo) na Mbeya (Usangu).

Mfumo wa uendeshaji wa ranchi za NARCO ni wa aina mbili; vitalu mama vinavyoendeshwa moja kwa moja na Kampuni na vitalu vinavyoendeshwa na wawekezaji wazawa. Kwa mantiki hiyo, NARCO inashirikiana bega kwa bega na sekta binafsi katika kuongeza kipato kupitia mifugo.

Mbari mahsusi ya ng’ombe inayofugwa na NARCO ni Borani. Hawa ni ng’ombe wakubwa, wastahimilivu na wenye kutoa nyama bora kabisa. Kwa NARCO nyama hii bora inaitwa Kongwa Beef. Tafadhali jipatie kipande chako cha nyama hii bora kutoka katika maduka yetu mbalimbali yaliyopo Kongwa ranchi (njia kuu ya Moro – Dodoma), Dodoma mjini (Area C), Dar es Salaam (Nkrumah Street), Ruvu ranch (njia kuu ya Dar – Morogoro), Morogoro mjini, Sanya Juu na Sumbawanga mjini. Tafuna kipande cha Kongwa Beef leo, na hutaicha kamwe!

Karibu NARCO, karibu tukuhudumie

Bw.Mohamedi Zuberi Mbwana

Mkurugenzi Mtendaji